Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hassan Rashid Jawad Al-Abayiji, Mkurugenzi wa Ataba Tukufu ya Imam Hussein (as), wakati wa Kongamano la Tano la Kimataifa la “Nidaa al-Aqsa” lililofanyika Karbala, alisisitiza kuwa; Harakati ya Imam Hussein (as) ni mradi wa milele wa mageuzi unaolenga kupambana na dhulma na ujeuri. Alieleza kwamba; kadhia ya Palestina leo ndiyo mwendelezo hai wa ujumbe wa Imam Hussein (as) katika kuwanusuru wanaodhulumiwa na kuutetea ukweli.
Alitoa wito wa kupata msukumo kutoka katika misingi ya Karbala katika njia ya kusimama imara, kujitolea na kupambana na aina zote za udikteta na ukoloni. Mkurugenzi wa Ataba Tukufu ya Imam Hussein (as) alisema katika hafla hiyo: “Sekretarieti ya Ataba Tukufu ya Imam Hussein (as), chini ya uongozi wa mwakilishi wa Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Sistani, Hujjatul Islam wal-Muslimin Sheikh Abdul Mahdi Al-Karbala'i, inawakaribisha kwa heshima katika kongamano hili lenye baraka, ambalo limefanyika sambamba na siku za matembezi ya Harakati ya Imam Hussein (as) kwa ajili ya ziara ya Arubaini.”
Aliongeza: “Kufanyika kwa kongamano hili kunatufanya kutafakari msimamo wa Uislamu na madhehebu ya Ahlul-Bayt (as) kuhusu dhulma na madhalimu; jambo ambalo lina umuhimu mkubwa. Ndani ya Qur'ani Tukufu kuna aya nyingi zinazozungumzia hatima ya matwaghuti, madhalimu na majabari, zikisisitiza kwamba sehemu kubwa ya adhabu za duniani ni matokeo ya dhulma na uonevu wanaoufanya watawala waovu dhidi ya wanadamu, hususan mataifa yaliyodhulumiwa.”
Al-Abayiji, akirejelea ahadi ya Mwenyezi Mungu, alisema: “Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu haghafiliki na yale wanayoyafanya madhalimu na majabari. Aya za Qur'ani zinawapa watu matumaini na utulivu kwamba nusura ya Mwenyezi Mungu ni ya hakika, Mwenyezi Mungu atawaokoa wanaodhulumiwa, atawarejeshea haki zao na atawaadhibu maadui duniani na Akhera kwa aina mbalimbali za adhabu, kama alivyoyaadhibu mataifa ya zamani yaliyokuwa ya kidhalimu ili yawe fundisho kwa wengine.”
Mkurugenzi wa Ataba Tukufu ya Imam Hussein (as) alisisitiza: “Lau isingekuwa Harakati ya Imam Hussein (as), Umma usingeamka, na katika Uislamu pasingesalia isipokuwa jina tu, na katika Qur'ani pasingesalia isipokuwa desturi tu. Imam Hussein (as) aliibeba bendera ya mageuzi, kuamrisha mema, kukataza maovu na kung'oa utawala wa mafisadi. Harakati hii haikuathiri tu wakati wa tukio la Karbala, bali imeendelea kuwa na athari katika zama zote kwa kuwa ilidhihirisha maana za uadilifu, uhuru, haki na kusimama mbele ya madhalimu.”
Aliendelea kusema: “Imam Hussein (as) si shujaa wa Karbala pekee, bali ni alama ya milele ya kukataa fedheha na batili. Wajibu wetu leo hauishii kwenye kulia na kuhuzunika; tunapaswa kuifahamu harakati hii na kupata msukumo kutoka kwake ili tuwe na mchango halisi katika jamii yetu.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake kuhusu Palestina alisema: “Kadhia ya Palestina ni mwendelezo wa Harakati ya Imam Hussein (as), mauaji na uharibifu unaofanywa kwa mpango na adui mhalifu wa Kizayuni mbele ya macho ya mashirika ya kimataifa na ulimwengu wa Kiislamu unaotazama kimya ni doa la aibu katika paji la uso wa ubinadamu.”
Akiwahutubia ndugu wa Kipalestina alisema: “Leo tunawaambia ndugu zetu wa Palestina: shikamaneni na Harakati ya Imam Hussein (as), kwani ndiyo itakayowafungulia njia na kuamsha mshikamano wa mataifa pamoja nanyi. Hakuna aliyeshikamana na harakati hii akakata tamaa, tunaamini kwamba ushindi wa kadhia ya Palestina unapatikana kwa kufuata njia ya wajukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww), na mbele ya yote ni Harakati ya Imam Hussein (as).”
Macho ya Waislamu huru yameelekezwa kwenye maeneo yao matakatifu, na kamwe hawatasalimu amri mbele ya ujeuri
Hassan Rashid Jawad Al-Abayiji aliendelea kusema katika Kongamano la Tano la Kimataifa la “Nidaa al-Aqsa”: “Leo tunauhutubia ulimwengu mzima na kutangaza kwamba; Palestina na Quds ni mahali pa Mtume Mtukufu (saww) ambapo Mwenyezi Mungu amepabariki, kutoka katika mji wa heshima, ngome ya waliodhulumiwa na wanamapinduzi, na Qibla ya watu huru; yaani mahali ulipopumzishwa mwili mtukufu wa Sayyid al-Shuhada Imam Hussein (as), kipenzi cha Mtume Mtukufu (saww), tunaungana kwa hisia na ndugu zetu wa Palestina kwa sababu ya maumivu, mateso, kufukuzwa makwao na mzingiro waliowekewa.”
Alisisitiza: “Kwa mwito huu tunatangaza kwamba macho ya Waislamu wa kweli yataendelea kuelekezwa kwenye maeneo yao matakatifu maadamu wana uhai, na kamwe hawatainamisha vichwa vyao mbele ya ujeuri, dhulma na miradi ya kuwasalisha na kuwafanya wanyenyekee.”
Mkurugenzi wa Ataba Tukufu ya Imam Hussein (as) alisema: “Kwa msaada wa Mola wa mbingu na ardhi, tuna imani kwamba tukishikamana na vizito viwili, yaani Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul-Bayt watoharifu kutoka katika kizazi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww), haki hii itawarejea wenyewe.”
Mwishoni mwa hotuba yake, Al-Abayiji alibainisha: “Hii ndiyo njia na msimamo ambao Marjaiyya ya Juu ya Kidini nchini Iraq, Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali al-Husayni Sistani, amekuwa akiitilia mkazo na kuifanyia kazi kwa ajili ya kuwanusuru wanaodhulumiwa na kuyakomboa maeneo matakatifu kutokana na uchafuzi wa maadui.”
Maoni yako